Uchumi
Jump to navigation
Jump to search
Uchumi ni jumla ya shughuli zote za binadamu zinazolenga kutosheleza mahitaji yao. Ni hasa uzalishaji, usambazaji na utumiaji wa bidhaa pamoja na kutolewa kwa huduma kwa njia mbalimbali.
Uchumi mara nyingi hutazamwa kwenye ngazi za kijiji, eneo, taifa au dunia.
Sayansi ya Uchumi (kwa Kiingereza economics) ni tawi la elimu inayochunguza masharti ya uchumi kufaulu au kushindwa.
Sekta za uchumi[hariri | hariri chanzo]
Uchumi wa jadi katika nchi nyingi ulikuwa hasa kilimo cha kujikimu pamoja na biashara ya kubadilishana bidhaa kadhaa zenye thamani kubwa. Kwa mfano, tangu kale migodi ya Zimbabwe ilichimba dhahabu iliyopelekwa baadaye hadi Asia na kando ya Mediteranea.
Katika uchumi wa kisasa mara nyingi sekta tatu hutofautishwa:
- Sekta ya msingi: kutoa na kuzaa malighafi pamoja na mazao katika mazingira asilia. Mifano ni kilimo, uchimbaji wa madini, uvuvi au kuvuna ubao.
- Sekta ya pili: shughuli za kubadilisha malighafi hizi kuwa bidhaa. Madini ya chuma hubadilishwa kuwa feleji; feleji hutumiwa na viwanda kutengeneza vyuma vya ujenzi, magari, vifaa vya nyumbani. Viwanda vya nguo hutumia pamba kutoka mashambani na kuibadilisha kuwa uzi halafu kitambaa na nguo.
- Sekta ya tatu: biashara au usambazaji wa bidhaa hizi kwa wateja pamoja na kuwatolea huduma. Mifano ni maduka yanayouza bidhaa zilizotengenezwa viwandani. Mingine ni huduma kama benki, hoteli, sinema na usafiri.
- Wataalamu wengine hutaja sekta ya nne: shughuli za kusambaza habari na pia utafiti wa teknolojia mpya unaoendelea kuwa muhimu katika nchi zinazoendelea. Wengine huingiza pia elimu (kazi za shule na vyuo) katika sekta hii ya uchumi.
Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]
- Mafunzo ya uchumi huria na bure kutoka MIT
- Vitabu kuhusu uchumi toka Wikibooks
- Majarida kuhusu uchumi mtandaoni
Makala hii kuhusu mambo ya uchumi bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Uchumi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |