Afyuni

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Shamba la mpopi chanzo cha afyuni
Afyuni bichi kutoka nchini Afghanistan

Afyuni (Kar. أفيون) ni dawa asilia inayopatikana kutokana na utomvi uliokauka wa maua aina ya mpopi (Papaver somniferum - Kiing.opium poppy). Ndani yake kuna kemikali mbalimbali ambazo ni kati ya madawa makali kabisa yenye uwezo wa kutuliza maumivu lakini zinasababisha pia ulevi unaozoesha watu haraka na kuwafanya wasiweze kuacha ulevi huu.

Yaliyomo

Uwezo na hatari za afyuni [hariri]

Afyuni hutuliza maumivu, kuondoa mikakamao, inapunguza njaa na husimamisha kuhara. Inasababisha pia ndoto rohoni zinazopendwa na watu na kutokana uwezo huu afyuni ina hatari ya kuzoesha watu kwa matumizi yake.

Ikitumiwa mno inaweza kuua watu wanaoacha kula chakula au kwa kusimamisha kazi ya mapavu. Hatari zake ni hasa upande wa kiroho kwa sababu watu wanategemea matumizi yake hawawezi kuiacha tena. Inapunguza uwezo wa akili na kunia kitu na kufuatilia mipango.

Siku hizi afyuni hutumiwa hasa kwa kutoa kemikali ndani yake na kutengeneza madawa kama morfini na heroini yanaoytumiwa kama madawa ya tiba lakini zaidi kama madawa ya kulevya ambayo ni hatari na haramu kote duniani yakitumiwa nje ya tiba.

Mavuno ya afyuni [hariri]

Tumba la mpopi limekatwa na utomvi mweupe unatoka nje; baada ya masaa utaganda kuwa kama mpira kahawia-nyeusi

Utomvi wa mpopi ni majimaji meupe yanayoganda haraka hewani kuwa dutu yenye rangi kahawia-nyeusi inayofanana na mpira. Katika hali hii huitwa afyuni bichi ilitumiwa tangu kale kama dawa la kutuliza maumivu likawezesha waganga wa wa Wahindi, Wachina na Waroma wa Kale kutekeleza upasuaji kwa watu. Pamoja na matumizi haya ilijulikana pia kama dawa la kulevya lakini hii ilikuwa matumizi ya pembeni tu hadi karne ya 15 BK.

Tangu karne ya 15 nchini China watu walianza kutumia afyuni bichi kama dawa la burudani wakilenga kwa ulevi wake. Lakini matumizi haya yalipatikana mara hache tu kutokana na uhaba na gharama za afyuni huko.

Historia ya usambazaji wake kama dawa la kulevya [hariri]

Ndio Waingeerza walioanza kulima mpopi na kutengeneza afyuni kwa wingi katika koloni yao huko Uhindi walipoona soko lake huko China. Wakasambaza afyuni kwa bei ndogo katika nchi nyingi za Asia hasa China. Upatikanaji huu wa afyuni ulisababisha matumizi yake na watu wengi waliozoeleshwa nayo na kuitegemea.

Serikali ya China iliona hasara ya biashara hii kwanza kwa sababu ya hatari kwa afya ya wananachi pili kwa sababu za hasara kwa uchumi kutokana na watu kupotea muda kwa ulevi na pia gharama za kununua afyuni kutoka nje. Serikali ilipokataa kuingizwa kwa afyuni Uingereza ilishambulia China katika vita ya afyuni (1840 na tena 1858) ikailazimisha kukubali biashara hii. Mwaka 1912 robo ya wanaume wote nchini China walitegemea matumizi ya afyuni ya mara kwa mara. Tatizo hili liliendelea hadi kukomeshwa kwa biashara yake chini ya utawala wa wakomunisti wa Mao Dzedong.

Baada ya vita kuu ya pili ya dunia matumizi ya afyuni yalipungua lakini matumizi ya madawa yanayotolewa ndani yake kama heroini yamezidi duniani.

Mengineyo [hariri]

Nchini Uturuki kuna mji wa Afyonkarahisar lililopata jina lake kutokana na kilimo cha mipopi na utengenezaji wa afyuni.