Makaa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta

Kwa fueli inayochimbwa ardhini tazama makaa mawe

Kuni inapangwa kwa rundo inayofunikwa baadaye kwa udongo
Makaa ya kuwaka

Makaa ni dutu mango yenye kiwango kikubwa cha kaboni inayotumiwa kama fueli. Kwa kawaida inapatikana kwa kupashia moto kuni na kuzia hewa isiingie. Ni fueli muhimu kwa watu wengi katika nchi za Afrika. Ilikuwa chanzo cha nishati ya kupikia na kupashia moto katika nchi nyingi za dunia kabla ya makaamawe kusambaa kwa rahisi zaidi tangu upatikanaji wa usafiri wa kisasa kama treni na meli.

Makaa huwa na faida juu ya kuni hasa kutokana kiwango kikubwa cha nishati ndani yake kulingana na uzito na mjao wake. Faida nyingine ni ya kwamba inawaka bila ulimi wa moto.

Kwa hiyo matumizi yake yameongezeka kwenye miji iliyo mbali na misitu kutokana na gharama za kusafirisha mizigo. Matumizi ya makaa yalisababisha uharibifu wa misitu katika nchi nyingi.

Makaa hutengenezwa kwa kupanga kuni kavu kama rundo na kuifunika kwa udongo bichi. Kuni inachomwa chini lakini udongo huzuia kuwaka kwake hivyo joto la ndani linaangamiza nyevu wa kuni na gesi zote zilizomo ndani ya kuni na kulisha ulimi wa moto. Inayobaki ni karibu kaboni tupu yenye mashimo nyingi ndani yake yanayosaidia kushika moto baadaye wakati makaa inawashwa.