Kimondo
Vimondo (pia: meteori au meteoridi) ni magimba madogo ya angani yanayozunguka jua. Yanaweza kuangukia duniani yakionekana kama moto angani.
Yaliyomo
Ukubwa
Ukubwa wa kimondo ni kuanzia punje ya mchanga hadi kufikia kipenyo cha mita kadhaa. Hivyo kimondo ni kidogo kuliko asteoridi na kikubwa kushinda vumbi la angani.
Kugonga angahewa ya dunia
Obiti ya kimondo unaweza kuingiliana na obiti ya dunia au sayari nyingine. Kimondo kikilikaribia gimba la angani kubwa zaidi kinavutwa nalo.
Kikikaribia mno dunia yetu kinaingia katika angahewa na kuanguka chini kwa kasi kubwa sana. Njiani kinapashwa moto kutokana na msuguano wa hewa dhidi yake. Kiasi cha joto kinatosha kuchoma kabisa kimondo kidogo hewani. Hii inaonekana kwa macho matupu kama mstari wa moto angani. Kama kimondo ni kikubwa zaidi ni sehemu zake za nje tu zinazochomwa na kiini kinagonga uso wa dunia.
Kati ya vimondo kumi vikubwa kabisa duniani ambavyo mabaki yake yanaonekana, kimojawapo ni Kimondo cha Mbozi nchini Tanzania.
Hatari za vimondo ?
Vimondo ni hatari kwa vyombo vya angani kwa sababu ya kasi yake kubwa. Hata punje ndogo yaweza kusababisha uharibifu mwingi.
Duniani kuna pia hatari fulani lakini si kubwa hali halisi. Katika miaka yote ya karne ya 20 kuna taarifa 21 pekee za nyumba kugongwa na kimondo.
Katika karne ya 20 kuna taarifa zifuatazo kuhusu watu walioathiriwa na vimondo:
- 5 Septemba 1907 Weng-li, China - familia yote kufa
- 30 Juni 1908 Tunguska, Siberia - moto porini, watu wawili kufa
- 28 Aprili 1927 Aba, Japan - binti kujeruhiwa
- 8 Desemba 1929 Zvezvan, Yugoslavia - kimondo kugonga kwenye arusi, mmoja kufa
- 16 Mei 1946 Santa Ana, Meksiko - nyumba kuharibiwa, watu 28 kujeruhiwa
- 30 Novemba 1946 Colford, Ufalme wa Muungano - simu kuharibiwa, mvulana kujeruhiwa
- 28 Novemba 1954 Sylacauga, Alabama, USA - kimondo cha kilogramu nne kugonga nyumba, mama kujeruhiwa
- 14 Agosti 1992 Mbale, Uganda - vimondo 48 kuanguka, mvulana kujeruhiwa
Mgongano na vimondo vikubwa
Mbali na hayo, kuna hatari moja kubwa kwa uhai wote duniani. Wataalamu huamini ya kwamba kila baada ya miaka elfu kadhaa hadi laki kadhaa kimondo kikubwa au zaidi asteroidi inaweza kugonga dunia. Nishati ya mgongano wa aina hii inaweza kuwa kubwa sana na kuleta uharibifu mwingi.
Tokeo la Tunguska tarehe 30 Juni 1908 katika pori la Siberia liliangusha miti milioni 60 kwenye eneo la kilomita za mraba 2000. Wataalamu walio wengi huamini ya kwamba lilisababishwa na kimondo. Kama lingetokea juu ya mji wa kisasa kungekuwa na vifo vingi sana.
Kuna pia kasoko kadhaa zilizosababishwa na vimondo. Vimondo vikubwa sana vilivyoweza kusababisha kasoko kubwa vinatokea kila baada ya miaka milioni kadhaa. Lakini vina hatari ya kuua kiasi kikubwa cha viumbe vyote katika nchi au hata katika dunia nzima.
Viungo vya Nje
- Kimondo cha Mbozi (Kijerumani)
- Ujurasa mzuri juu ya vimondo kutoka Kanada
- Hatari za vimondo
- Matokeo ya migongano na vimondo
Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Kimondo kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |